
Taarifa ya Pamoja kwa Siku ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Umma - 23 Juni 2025 - katika mkesha wa Kongamano la 4 la Umoja wa Mataifa la Ufadhili wa Maendeleo
Chini ya moja ya tano ya malengo ya maendeleo endelevu yaliyowekwa miaka kumi iliyopita kwa sasa yanakaribia kufikiwa mwaka wa 2030. Sababu kuu ya hii ni ufadhili duni wa huduma za umma kote ulimwenguni. Robo tatu ya nchi za kipato cha chini hutumia fedha zaidi kulipa madeni kuliko afya, na nusu ya nchi hizi hutumia fedha zaidi kulipa wadai matajiri kuliko wanavyotumia kwa elimu. Ukosefu wa haki na usawa katika sheria na kanuni za kimataifa za kodi na biashara unachangia mtiririko endelevu wa rasilimali zinazohitajika kwa dharura kutoka Kusini mwa Dunia. Wakati huo huo, sera ya IMF bado ni kulazimisha nchi mbalimbali kubana matumizi katika huduma za umma na hivyo kudhoofisha mapambano dhidi ya umaskini na ukosefu wa usawa. Lakini yote haya yanaweza na lazima yabadilike!
Mwaka huu, Siku ya Huduma za Umma inaangukia wiki moja tu kabla ya Mkutano wa 4 wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo (FFD4). Mkutano huu wa Umoja wa Mataifa unaandaliwa huko Seville - jiji linalohusishwa kwa karibu na ukoloni wa Amerika ya Kusini – hata hivyo unatoa nafasi bora zaidi katika kizazi hiki cha kurekebisha na kuondoa ukoloni katika usanifu wa kifedha wa kimataifa. Jambo hili ni muhimu ikiwa mataifa yatabadilisha miongo kadhaa ya kupunguza bajetina kuanza kufadhili kikamilifu huduma za umma kwa wote, zinazoleta uhaki na usawa wa kijinsia.
Huku nchi 54 sasa zikikabiliwa na mgogoro wa madeni, ni wazi kuwa kufutwa kwa deni kunahitajika haraka ikiwa nchi zitagharamia ipasavyo huduma bora za umma. Vile vile, katika mwaka huu wa msamaha wa madeni wa Jubilei, kufutwa kwa madeni ni muhimu, haitoshi. Zaidi ya dola bilioni 100 za madeni zilifutwa mwaka 2005, lakini bila mabadiliko yoyote yaliyokubaliwa kwa mfumo usio wa haki wa kifedha uliosababisha mgogoro huo, nchi nyingi za kipato cha chini leo zinajikuta zinakabiliwa na mgogoro mpya, mkali zaidi. Kwa hivyo, 2025 lazima iwe mwaka ambao usanifu wa kimataifa kuhusu deni unabadilishwa kupitia kuanzisha Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Madeni ya Kitaifa, kutengeneza mikataba mapya ya kimataifa kuhusu uwajibikaji wa mikopo na ukopaji, na kuhamisha mamlaka juu ya deni kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) hadi shirika la Umoja wa Mataifa. Mabadiliko haya ni muhimu kuwezesha nchi kuwa na rasilimali za kuboreshahuduma za umma. Kurekebisha mfumo wa madeni wa kimataifa ni moja kati ya madai ya msingi ya mataifa ya Afrika na mashirika yasiyo ya kiserikali zinazofuata mada hii ya FFD4 - lakini unazuiwa na nchi tajiri na wadai wa kibinafsi ambao wanafaidika kutokana na udhalimu wa mfumo huu.
Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi unaongeza hali ya dharurakatika muktadha wa mageuzi ya kimsingi ya mfumo wa ufadhili, ili nchi ziweze kuwekeza katika huduma za umma huku wakizingatia mabadiliko ya haki zaidi, usawa, uendelevu na ushirikishwaji. Sasa ni wazi kwamba mgogoro wa madeni umeunganishwa kwa karibu na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchiwhats , huku nchi zenye madeni zikilazimika kupata fedha za kigeni haraka na hivyo kulazimika kuwekeza katika uchimbaji wa mafuta na kilimo cha viwanda - sababu mbili kubwa za mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi. Kwa upande mwingine, nchi ambazo ziko hatarini zaidi kwa mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi zinachukuliwa kuwa nchi nchi zilizo katika 'hatari kubwa' kwa uwekezaji, na hivyo hutozwa viwango vya juu vya riba kwa mikopo (hasa baada ya majanga yanayotokana na mabadiliiko ya hali ya hewa), kuharakisha uwezekano na ukubwa wa migogoro ya madeni. Lakini lazima tuangalie taswira kubwa ya deni na kuuliza, nani anamdai nani? Uchambuzi wa hivi punde unaonyesha kuwa nchi tajiri zinazotoa moshi mwingi katika Ukanda wa Kaskazini mwa Dunia zina deni kubwa la mabadiliko ya tabianchi kwa nchi za kipato cha chini, kwa kujimilikisha rasilimali ya pamoja ya angahewa (kuchafua sayari na kusababisha mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi). Kwa bahati mbaya, hakuna mfumo wa kimataifa wa kuaminika wa kulazimisha ulipaji wa madeni haya ya tabianchi - ambayo ni makubwa zaidi kuliko madeni ya nje yanayotekelezwa kikatili dhidi ya nchi za kipato cha chini. Hili lazima libadilike, kupitia mageuzi ya mfumo wa kimataifa na ahadi kutoka kwa nchi tajiri ya kutoa fedha za tabianchi kwa ajili ya kulipa madeni haya ya tabianchi - ambayo lazima yaje kwa njia ya ruzuku (sio mikopo kwa nchi ambazo tayari zinadaiwa) - kwa ahadi ya kuunga mkono mabadiliko ya haki kulingana na mifumo ya umma inayofadhiliwa kwa fedha za umma.
Katika kilele cha mfumo wa kifedha usio na haki uliopo, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). IMFinaendeleza utaratibu wa kiuchumi wa kimataifa unaopendelea makampuni ya kimataifa, wadai na mataifa tajiri, huku wakifunga nchi za kipato cha chini katika mizunguko katili na inayojirudia ya deni na utegemezi. Inakadiriwa kuwa kwa kila dola moja ya Marekani ambayo IMF imehimiza serikali kutumia katika huduma za umma, imewaambia kupunguza mara sita zaidi kupitia hatua za kubana matumizi. Utaratibu wa uendeshaji wa IMF ulianzishwa wakati wa Mipango ya Marekebisho ya Miundo ya miaka ya 1980, wakati iliweka ubanaji mkubwa wa matumizi ya umma katika mataifa ambayo yalikuwa yamechukua mikopo. Nyingi za nchi hizi zilikuwa zimejipatia uhuru hivi majuzi kutoka kwa nchi zilezile zinazoidhinisha IMF. Leo, matamshi yamebadilika, lakini IMF inaendelea kutekeleza ajenda yake ya kubana matumizi kwa vitendo, na kusababisha kupunguzwa mara kwa mara na kufungia malipo ya mishahara katika sekta ya umma , hata katika nchi zilizo na uhaba mkubwa wa wafanyikazi wa sekta ya umma. Huku huduma za umma zikiachwa zikiwa na ufadhili wa chini, serikali zinaendelea kushinikizwa katika ufanyaji biashara, ubinafsishaji na Ushirikiano wa Umma na Kibinafsi (yani PPP) unaopea faida kipaumbele kuliko watu.
Sehemu ya mabadiliko ya mfumo ambayo inahitajika ili kubadilisha huduma za umma inahusiana na haki ya kodi . Marekebisho ya kodi yenye malengo makubwa na yenye kuzingatia uwezo wa mlipakodi yanahitajika kwa dharura katika ngazi ya kimataifa, kitaifa na ndani. Mmomonyoko wa msingi wa kodi, ubadilishaji wa faida, na ukwepaji wa kodi huzuia serikali, na zile za Kusini mwa Ulimwengu hasa, kukusanya mapato ya ndani ambayo ni muhimu ili kufadhili huduma za umma kwa uendelevu. Ili kufanya maamuzi ya kimataifa kuhusu kodi kuwa sawa na kuwezesha nchi kupitisha mageuzi ya kodi katika ngazi ya ndani, unapaswa kuondokana na mapungufu ya kidemokrasia ya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD). Kwa miaka 60, OECD imeweka sheria za ushuru duniani zinazowakilisha maslahi ya nchi tajiri, hasa makampuni na watu tajiri. Kufuatia utetezi wenye mafanikio wa mataifa ya Afrika katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, sasa kuna makubaliano ya kuandaa Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ushirikiano wa Kimataifa wa Masuala ya Kodi, ambao unaweza kuanzisha mfumo wa kimataifa wa usimamizi wa kodi ulio wazi zaidi, wenye usawa na unaowajibika na utakaonufaisha mataifa yote. Tunaunga mkono kikamilifu maendeleo kwenye mkataba huu na lazima tuhakikishe kwamba mkutano wa FFD4 hauhujumu mchakato huu uliopo kwa njia yoyote ile. Pia tunaunga mkono hitaji la kuendeleza uongozi wa kihistoria wa Brazili katika G20 mwaka jana ambao uliweka ushuru wa utajiri wa watu matajiri zaidi kwenye ajenda ya kimataifa.
Mnamo 2025, tunaona upungufu mkubwa wa bajeti ya misaada kutoka Marekani, Uingereza na mataifa mengi ya Ulaya, pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya kijeshi. Nchi tajiri zinaonekana kutaka kujitenga badala ya kujenga madaraja. Wakati huo huo, imekuwa wazi zaidi kwamba sekta binafsi haiwezikuziba mapengo! Mbinu ya "mabilioni hadi matrilioni ", ambayo ililenga kutumia fedha za umma kufungua uwekezaji wa kibinafsi katika nchi zinazoendelea, haijafanikiwa kwa kiasi kikubwa, na ilishutumiwa hivi karibuni hata na Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia . Kinachohitajika kwa haraka ni udhibiti thabiti wa umma wa watendaji binafsi na serikali imara, inayowajibika na inayoongoza katika kufadhili na kutoa huduma bora za umma. Tena, hii inaongeza udharura wa haja ya mageuzi ya kimataifa ili kurudisha nyuma dhuluma ya madeni, dhuluma ya kodi na sera za kubana matumizi, na kujenga msingi wa mataifa yanayoweza kuheshimu, kulinda na kutimiza haki za binadamu. Utashi wa kisiasa wa ndani na hatua za kitaifa vitahitajika kila wakati, lakini katika mfumo wa sasa wa kimataifa usio wa haki, mataifa yote yanajitahidi kufadhili huduma za umma kwa wote.
Kwa bahati nzuri, kuna kasi mpya ya kimataifa ya kutetea uboreshaji wa fedha za umma na huduma za umma. Mwishoni mwa 2022, zaidi ya wawakilishi elfu moja kutoka zaidi ya nchi mia moja walikusanyika Chile chini ya bendera ya 'Mustakabali Wetu ni wa Umma '. Azimio la Santiago la Huduma za Umma liliweka ajenda ya pamoja kutoka kwa vyama vya wafanyakazi, mashirika na vuguvugu zinazoshughulikia huduma mbali mbali za umma, zikiwemo elimu, afya, matunzo, nishati, chakula na lishe, makazi, maji, usafiri na hifadhi ya jamii. Tulipaza sauti zetu dhidi ya ubiasharishaji na ubinafsishaji unaodhuru haki, kwa kutambua ya kwamba mambo haya yamesababisha kuongezeka kwa ukosefu wa usawa na ukosefu wa haki. Kwa pamoja tulikosoa miundo na mawazo ya kikoloni ambayo yanaendelea kusababisha ufadhili duni wa huduma za umma. Na tulilaani mfumo wa sasa wa kifedha wa kimataifa ambao unaweka idadi kubwa ya watu duniani katika umaskini.
Ni lazima Mkutano wa FFD ujitolee kwa mkataba mpya wa kijamii unaohakikisha mfumo wa fedha wa kimataifa unaotanguliza watu na sayari mbele ya faida, na ambao unayawezesha mataifa kutoa huduma za umma kwa wote na hifadhi ya jamii kwa kila mtu. Tunasisitiza kwamba kuna njia mbadala za wazi kwa hali ilivyo sasa, nyingi zimewekwa katika Manifesto ya Kimataifa ya Huduma za Umma , Ilani ya Kujenga Upya Mpangilio wa Kijamii wa Malezi, na Mustakabali Wetu ni wa Umma: Tamko la Demokrasia ya Nishati . Tunatoa wito kwa utambuzi wao na marekebisho ya mfumo wa kifedha wa kimataifa uliopitwa na wakati.
Katika siku hii ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Umma, tunaungana tena kusisitiza wito wetu wa mustakabali wa umma. Wiki ijayo huko Seville, tunahitaji serikali ziwe na ujasiri wa kukubaliana kuhusu tamko la mwisho litakalobadilisha kwa kweli mfumo dhalimui wa ugharamiaji,ili kuharakisha maendeleo kuelekea huduma bora za umma kwa kila mtu, popote alipo.
IMETHIBITISHWA NA:
Action against Hunger France
ActionAid International
Africa Network Campaign on Education for All (ANCEFA)
Amnesty International
Arab Campaign for Education for All (ACEA)
Arab Network for Popular Education (ANPE Lebanese Coalition)
Asia South Pacific Association for Basic and Adult Education (ASPBAE)
Brazilian Campaign for the Right to Education
Bretton Woods Project
Campaña Latinoamericana por el Derecho a la Educación-CLADE
Center for Economic and Social Rights (CESR)
Education International
eduCoop
Enginyeria sense Fronteres
Enginyeria sense Fronteres
Eurodad
Global Campaign for Education (GCE)
Global Initiative for Economic, Social and Cultural Rights (GI-ESCR)
Global Social Justice
Institute for Economic Justice
International Association for Hospice and Palliative Care
National Campaign for Education Nepal (NCE Nepal)
Network for Education Watch (NEW) Indonesia
Oxfam
Paropakar Primary Health Care Centre PPUK
Public Services International (PSI)
Right to Education Initiative
RTE Forum, India
Society for International Development (SID)
Solidarité Laïque
Tax and Education (Tax Ed) Alliance
Tax Justice Network
The Alternatives Project (TAP)
Transnational Institute (TNI)
World Organization for Early Childhood Education – OMEP