PSI-Mwongozo wa Mabadiliko ya Tabianchi Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi: Ni Muda Wa Vitendo
Wakati janga la virusi vya korona linapoendelea kuuandama ulimwengu, miji imekuwa rafiki zaidi kuishi, hali ya hewa imekuwa safi, hali ya kelele imepungua na kuwa yenye kuvumilika. Lakini, gharama iliyolipwa kwa ajili ya faida hizi ni kubwa ikiwemo: kupoteza kipato na ajira na kuwepo kwa hali kubwa ya wasiwasi, taharuki na huzuni.
Tunapozindua Mwongozo wa Mabadiliko ya Tabianchi, sehemu kubwa ya ulimwengu bado ipo kwenye zuio la kutotoka nje kutokana na janga la virusi vya korona, huku baadhi wakiwa kwenye harakati za kuzoea uhalisia mpya na mgumu zaidi. Hali hii inatoa kwa PSI na washirika wake fursa na changamoto nyingi, ambazo zinahitaji maandalizi.
Ipo haja ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa asilimia 7 kila mwaka. Hiki ni kiashirio kuwa hatupaswi kuendelea na maisha ya kila siku kama tuzivyokuwa tumezoea
Wanasayansi wametabiri kuwa uzalishaji wa hewa chafu utapungua kwa asilimia 5 kuanzia mwaka 2020 ikilinganishwa na mwaka 2019. Hii inatokana na janga la virusi vya korona kupunguza shughuli za kiuchumi duniani. Hata hivyo, ili kubakia ndani ya lengo la nyuzi joto 1.5 kama ilivyo katika Makubaliano ya Paris, ipo haja ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu kwa asilimia 7 kila mwaka. Hiki ni kiashirio kuwa hatupaswi kuendelea na maisha ya kila siku kama tuzivyokuwa tumezoea. Tunapaswa kuchukua hatua madhubuti kubadilisha mifumo yetu ya uchumi na jamii zetu kwa ujumla.
Mwongozo huu wa mabadiliko ya tabianchi utasaidia vyama vya wafanyakazi kutengeneza na kuboresha mikakati ya kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi. Mazoezi yaliyowekwa kwenye mwongozo huu pamoja na maudhui ya ziada yanaweza kutumiwa na mfanyakazi mmoja mmoja au kwa ubora zaidi katika vikundi. Vyama vya wafanyakazi vitahitaji kutengeneza mikakati kwa kushirikiana na asasi za kiraia, viongozi wa kisiasa na wadau wengine kutoka nyanja tofauti tofauti.
Wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi wanaweza kuchukua hatua za moja kwa moja na haraka zaidi katika sehemu zao kazi. Sehemu za kazi zinaweza kuwa mahala pasipo zalisha hewa chafu na kutokuwa na athari kwenye mazingira. Shirika la PSI litaendelea kufanya uchambuzi wakisekta, kukusanya uzoefu na kutoa taarifa za mafanikio yaliyofikiwa kutoka kwa washirika wake. ITUC imezindua kampeni yenye kuhamasisha umuhimu wa ‘kufanya sehemu za kazi kuwa kijani’ na kuvitaka vyama vya wafanyakazi kutoa taarifa kila ifikapo tarehe 24 Juni ya kila mwaka. Tunahimiza vyama vya wafanyakazi kushiriki kikamilifu.
Bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kumaliza changamoto sugu ya mabadiliko ya tabianchi miongoni mwetu. Ni tumaini letu kuwa mwongozo huu utaongeza uelewa na kuwafanya watu wachukue hatua stahiki. Shirika la PSI litaanzisha jukwaa maalum kwa ajili ya washirika wake kutoa ujuzi na uzoefu. Pia jukwaa hili litaratibu shughuli zote zinazohusu mapambano ya mabadiliko ya tabianchi.